Tuesday, February 21, 2012

Mwenyekiti Wazazi (CCM) Tanga ajiunga Chadema

Na Peter Mwenda,Tanga

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata ya Maramo ya Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Muheza mjini na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Bw. Hassan Mrisho Mngazija amejiondoa chama hicho na kujiunga na Chadema.
Bw. Mngazija ni mmoja wa wanachama wapya zaidi ya 500 walikabidhiwa kadi mpya za kujiunga na Chadema katika mikutano ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara Bw. Zitto Kabwe katika mkoa wa Tanga.

"Akihutubia mikutano ya hadhara katika Wilaya ya Muheza, akiwa kwenye ziara ya kukagua uhai wa chama mkoani Tanga Bw. Zitto Kabwe alisema kuwa hali ya wananchi kukosa matumaini kwa watawala wao (CCM) ni moja ya dalili mbaya kwa utawala wowote ule na tishio kubwa la amani ya nchi.
Alisema iwapo hali ya wananchi kukosa matumaini inayojionesha miongoni mwa Watanzania kutokana na utawala mbovu usiojali matatizo yanayowakabili na kuacha hali hiyo iendelee bila kutafutiwa suluhisho, itakuwa ni hatari kwa watawala na mstakabali wa nchi.

Bw. Zitto alisema tabia ya viongozi kutowasemea wananchi wanyonge, hasa wale wa vijijini, chama hicho kimejitolea kuifanya kazi hiyo katika majukwaa mbalimbali, ikiwemo mikutano ya hadhara, bungeni na kokote kule, ambako kitaweza kupaza sauti kuonesha uongozi mbadala namna ambavyo nchi inapaswa kuongozwa, kikijikita kutoa suluhisho ya matatizo hayo.

“Wananchi mmepoteza matumaini, mmekata tamaa, hamuwaamini tena watawala walioko madarakani, mmepoteza matumaini na CCM. Kwa mambo mliyofanyiwa miaka nenda rudi na chama hicho, hamtuamini tena wanasiasa, kila anayekuja mnamuona ni yule yule, Kila mkitusikiliza mnatusikia tunazozana kuhusu posho, tunagombania maslahi yetu, badala ya kuwasemea ninyi wanyonge wenye nchi"alisema Bw. Zitto na kushangiliwa na umati wa wananchi walijitokeza kumsikiliza.
Alisema kati ya mambo ambayo yataipasua nchi hii ni suala la ukosefu wa ajira kwa vijana na ufisadi, rushwa na ubadhirifu upande mwingine.
Alisema miaka mitano sasa wananchi wamekuwa wakisoma katika magazeti na kusikia fulani kapiga pale, fulani kapiga hapa, mkurugenzi yule wa halmashauri kaiba pale, mkurugenzi huyu wa shirika la umma kaiba hapa na mengine ya wanasiasa mafisadi wanazidi kupoteza matumaini.

Bw. Zitto alisema matukio hayo yanawalea vibaya watoto  wa kitanzania Wataamini kuwa ukitaka kuishi katika nchi hii ni lazima uwe fisadi, kitu ambacho sikweli. Watawala sasa wanafikiria kula tu, wanafikiria maslahi yao, hawasemei tena wananchi maskini, hasa walioko vijijini. Tangu alipofariki Mwalimu Nyerere, aliyekuwa watetezi wa wanyonge, wananchi wa vijijini wamekosa msemaji kabisa,” alisema Zitto.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alitolea mfano wa namna wananchi wa vijijini walivyotelekezwa, akisema kuwa kila inapotokea umeme umekatika maeneo ya miji mikubwa, nchi husemwa ‘iko gizani’, bila kujali kuwa kuna wananchi tangu Tanzania ipate uhuru ‘wako gizani’ miaka yote, lakini athari za kukosekana kwa nishati hiyo ikiendelea kuwaathiri.

Mbali ya kukagua uhai wa chama mkoani Tanga, Zitto pia anafanya ziara mkoani Tanga, kwa ajili ya kuifafanua hoja yake juu ya zao la mkonge, aliyoiwasilisha bungeni katika mkutano wa bunge uliopita.
mwisho

No comments: